WAZIRI MAVUNDE AZINDUA TIMU YA MAJADILIANO WIZARA YA MADINI
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde leo tarehe 12 Machi, 2024 amezindua Timu ya Wizara ya Majadiliano katika Ukumbi wa Nishati, Jijini Dodoma.
Uzinduzi wa Timu hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Madini Sura ya 123 kinachohusu ushiriki wa Serikali katika umiliki wa Hisa katika Kampuni za Madini zinazomiliki Leseni za Kati na Leseni Kubwa.
Akizunguza katika uzinduzi huo, Waziri Mavunde ameitaka Timu hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuweka mbele maslahi ya nchi ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu ya Timu hiyo unaongeza mchango wa Sekta ya Madini katika uchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu hiyo Prof.Sifuni Mchome, amemshukuru Waziri kwa uteuzi wa Timu hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika uchumi wa nchi. Pia, Timu hiyo itahakikisha kuwa inalinda maslahi ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Timu hiyo ambayo muda wake ni miaka mitatu (3) inachukua baadhi ya majukumu ya Timu Maalum ya Serikali ya Majadiliano (SPGNT) iliyokuwa ikiongozwa na Prof. Palamagamba Kabudi.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mhe. Steven Kiruswa (Mb.), Naibu Waziri wa Madini, Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano, Profesa Sifuni Mchome, Makamu Mwenyekiti, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga, Wajumbe na Sekretarieti.