HAMASISHENI WANANCHI KUJIUNGA NA CHF – DKT. MFAUME
Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amezitaka Timu za Usimamizi na Uratibu wa shughuli za afya ,Lishe, na Ustawi wa Jamii ngazi ya Halmashauri (CHMT) kuhakikisha wananchi wanahamasishwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF iliyoboreshwa.
Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo mkoani Tabora alipotembelea na kukagua ufanisi wa watoa huduma za Afya katika Zahanati ya Lubisu iliyopo katika Halmashauri ya Nzega mkoa wa Tabora inapojengwa Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Nzega ambapo amebaini kutokuwepo kwa mwananchi ambaye amewahi kutibiwa katika kituo hicho kwa kadi ya CHF huku watoa huduma wakiwa hawana elimu kuhusu huduma hiyo.
“Zahanati nyingi hazijajengewa uwezo juu ya CHF na watendaji wa vijiji na kata hawajahamasishwa hawajashirikisha kwenda kuhamasisha jamii kujiunga na CHF mi nashangaa nakuja hapa kwenye kituo hata watumishi wenyewe hawajengewa uwezo na tumeambia kuna wateja zaidi ya elfu 20 wanakuja hapa na hakuna hata mmoja anakuja na kadi ya CHF tangu kituo kimefunguliwa hapa miaka mitatu iliyopita” amesema Dkt. Mfaume
Dkt. Mfaume amesema endapo wananchi watajiunga na mfuko huo itamsaidia mwananchi kupata huduma kwa gharama nafuu kwani gharama ya kadi hiyo ni shilingi elfu 30 ambapo mwananchi atapata huduma hiyo katika kituo chochote cha Afya nchini yeye pamoja na wategemezi wake kwa kipindi cha mwaka mmoja
Hata hivyo ameonesha kutoridhishwa na utendaji wa CHMT ya Halmashauri ya Nzega na ametoa muda wa wiki moja kuwasilisha kwa mkurugenzi wa Halmashauri mikakati ya kushirikisha viongozi wa ngazi ya jamii na elimu kwa watoa huduma wa Afya ili kuhamasisha wananchi kujiuna na mfuko huo.