WATAALAM MADINI, ASNL ADVISORY WAJADILI UANZISHWAJI WA MFUKO WA MADINI

0

Wataalam wa Wizara ya Madini wamekutana na Kampuni ya ASNL Advisory Limited kwa lengo la kujadiliana kuhusu uanzishwaji wa Mfuko wa Madini (Mineral Wealth Fund) ili kuwa na mfuko wa akiba, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, sambamba na kukabiliana na mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za madini katika soko la dunia.

Kikao hicho kilichofanyika leo Februari 27, 2024 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, kimeongozwa na Kamishna Msaidizi wa Madini Francis Mihayo.



Mihayo ameishukuru Kampuni ya ASNL Advisory Limited kwa wasilisho lao kuhusu uzoefu wa Nchi nyingine zilizo na mfuko huo na kusema kuwa wazo la kuanzishwa kwake litasaidia kukuza faida za muda mrefu za mapato ya madini kwa nchi na wananchi wake kwa miaka ijayo.

Amesema kuwa, wazo hilo litachakatwa zaidi na Wataalam wa Wizara kwa kuangalia mfumo wa kisheria unaohitajika kuanzisha na kusimamia mfuko kwa ufanisi, kuhakikisha sheria zinafuatwa, kuweka Mkakati wa uwekezaji wa mfuko kwa kutilia maanani mambo muhimu, muundo wa utawala wa mfuko, ikiwa ni pamoja na majukumu ya wadau, mchakato wa kufanya maamuzi na njia za uwajibikaji na uwazi.


Mihayo ameongeza kuwa, pia Wizara itajadili mikakati ya kutambua, kutathmini, na kupunguza hatari (risks) zinazohusiana na usimamizi wa mfuko, ikiwa ni pamoja na hatari za soko (market risks), hatari za uendeshaji (operational risks) na hatari zinazoweza kutokea (compliance risks).

“Tunaahidi kuendeleza ushirikiano na nyie (ASNL Advisory Limited) tunatambua utaalam na uwezo wenu katika kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu, kiufundi, na usimamizi ili kusaidia katika kuanzisha na kuendesha mfuko huu. Lakini wadau wengine kama Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha na taasisi binafsi pia tutashirikiana nao ili tupate muundo mzuri wa kuanzisha huu mfuko” amesisitiza Mihayo

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ushauri Mnyororo wa Ugavi kutoka ASNL Humphrey Simba amesema kuwa wazo hilo limekuwa wakilichakata tangu mwezi Machi 2023 na kuona ni kwa jinsi gani na wao wanaweza kushiriki katika ubunifu kwa manufaa ya taifa mbali na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu, kiufundi na usimamizi kwa anuwai ya viwanda vinavyoshiriki katika mnyororo wa thamani wa uchimbaji madini.

Awali, akifanya wasilisho Mkurugenzi wa Ushauri wa Fedha kutoka ASNL Patrick Nanyaro ameeleza kuwa, rasilimali madini haitachimbwa milele na kwa kuwa mfuko huo hujumuisha fedha ambazo mara nyingi hutokana na akiba ya ziada ya nchi na hutoa faida kwa uchumi wa nchi na raia wake basi manufaa yatakuwa makubwa akitolea mfano nchi ya Norway ambayo mfuko wake hivi sasa una thamani ya dola za Marekani trilioni 1.5.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *