BUNGE LASHAURI SERIKALI KUPELEKA FEDHA ZA KUTOSHA TARURA

0

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeishauri Serikali   kuona umuhimu wa kuipelekea fedha za kutosha TARURA   kwa kadiri ya bajeti  ilivyoainishwa  ili iweze kukabiliana  na hali mbaya ya miundombinu  nchini.

Ushauri huo umetolewa Bungeni leo Februari 13, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Mikumi Mheshimiwa Dennis Londo wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kipindi cha kuanzia Februari, 2023 hadi Januari, 2024

Amesema kamati haijaridhishwa na hali ya upelekaji wa fedha za bajeti kwa TARURA, ikizingatiwa kuwa katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo uharibifu wa miundombinu ya barabara nchini uliotokana  na mvua zinazoendelea kunyesha katika sehemu kubwa ya nchi.

“Ikumbukwe kuwa Serikali iliahidi ndani ya Bunge lako kuwa pamoja na bajeti ya Bilioni 808.02 Serikali ingetoa Bilioni 350 za ziada kwa TARURA. Kamati inasikitika kwamba, hata fedha hizi pia hazijapokelewa, hivyo tunaiomba Serikali iweze kutoa fedha kwa wakati ili kutatua changamoto za miundombinu nchini “ amesisitiza Mheshimiwa Londo.

Aidha, amesema Kamati imeiomba Serikali  kuhakikisha inaiongezea  bajeti TARURA  kufikia shilingi  trilioni 1.64 kutoka shilingi  bilioni 710 kwa miaka minne mfululizo ili kufikia malengo  ya asilimia 70 ya barabara  kuwa za changarawe, asilimia 3 kuwa  barabara za lami.

Pia, imeitaka  Serikali kuhakikisha inasimamia kwa umakini taratibu za manunuzi kulingana na uwezo wa wakandarasi wanaoomba kazi na utekelezaji wa miradi husika.

Vilevile, wameielekeza Serikali kutekeleza mchakato wa kuanzisha Hati Fungani (TARURA SAMIA INFRASTRUCTURE BOND) kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara pamoja na kutafuta vyanzo vya fedha mbadala ikiwemo kushirikisha sekta binafsi ili kuiwezesha TARURA kuwa na fedha za uhakika za kutekeleza miradi ya barabara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *