MLIMA KITONGA UMEANZA KUPANULIWA
Serikali imeanza upanuzi wa barabara kuu ya TANZAM kutokea Ruaha Mbuyuni hususan eneo la mlima Kitonga wenye urefu wa KM 7.6 kutoka njia mbili kwenda njia tatu sehemu zenye kona ili kuepusha msongamano wa mara kwa mara na hivyo kuwezesha eneo hilo kupitika kiurahisi wakati wote.
Meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa Mhandisi Yudas Msangi amesema ujenzi wa mradi huu utagharimu shilingi bilioni 6.4 ambapo kwa awamu ya kwanza itahusisha sehemu zenye kona wakati upembuzi yakinifu wa kuboresha eneo hilo kujengwa kwa njia nne au kwa handaki ukiendelea.
” kwa hatua ya sasa tunapanua sehemu za kona kali kwa upana wa mita 5, wakati tukisubiri upembuzi yakinifu ukamilike utakaoamua tujenge njia nne au tutoboe handaki ili kumaliza changamoto ya mlima Kitonga”, Amesema Eng. Msangi.
Ujenzi huo wa njia tatu sehemu za kona pia utahusisha mifereji mikubwa ya kuongoza maji na kufungwa vioo vikubwa kwenye kona ili kusaidia kupishana kwa magari nyakati zote .
“ Kwa sasa tunachonga mlima huu ili kupata usawa wa barabara na baada ya kukamilisha tutaanza kazi ya zege ambalo litakuwa na upana wa mita tano ili kuepusha utelezi mara baada ya Ujenzi kukamilika“ amesisitiza Eng. Msangi.
Ujenzi huo unafanyika kufuatia maelekezo ya Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa aliyoyatoa hivi karibuni alipokagua maendeleo ya barabara.