SERIKALI IMEWEKA KIPAUMBELE KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA – NDEJEMBI
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Deogratius Ndejembi amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha utoaji wa huduma za kiutawala, kiuchumi, kijamii kupitia ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa katika maeneo ya utawala yaliyopo ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa, Kata na vijiji na endapo kuna ulazima wa kuanzisha maeneo mapya, Serikali itatoa maelekezo muda muafaka utakapofika.
Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilombero mkoani Morogoro, Mhe. Abubakar Asenga katika kikao cha kwanza cha mkutano wa 14 wa Bunge la 12 lililoanza leo Januari 30 2024 jijini Dodoma.
Mhe. Asenga alihoji ni lini serikali itagawa Mkoa wa Morogoro na kupata mkoa mpya kama ilivyopendekezwa na mkoa huo.