Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki mazungumzo ya pande mbili (bilateral talks) na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Mtawala wa Dubai, Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, pembezoni mwa Mkutano wa World Government Summit (WGS 2026) mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Viongozi hao wamekubaliana kuendeleza mahusiano ya kiuchumi na kibiashara ikiwemo kukamilisha Mikataba ya Ushirikiano wa Biashara (CEPA) na Mikataba ya Uwekezaji wa Nchi na Nchi (BIT), ili kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na UAE.
Halikadhalika, wamejadili kuhusu utekelezaji wa miradi ya pamoja na uwezekano wa kuanzishwa kwa safari mpya za anga kwa Shirika la Ndege la Emirates, ikiwemo safari ya Kilimanjaro – Zanzibar, kwa lengo la kukuza utalii na biashara.
Kwa upande wake, Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kupitia miradi ya maendeleo kwa manufaa ya ustawi wa uchumi wa pande zote mbili.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameshiriki katika mjadala wa kimataifa kuhusu uwekezaji, katika Mkutano wa Jukwaa la Serikali Duniani (World Governments Summit 2026), uliofanyika leo tarehe 04 Februari, 2026, mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Mjadala huo wenye mada: “Serikali na Mustakabali wa Uwekezaji: Mtazamo wa Afrika,” ulilenga kujadili nafasi ya Serikali katika kuvutia mitaji na kukuza uchumi barani Afrika.
Rais Dkt. Samia amewasilisha uzoefu wa Tanzania katika kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kisheria, ikiwemo marekebisho ya sera, sheria na taratibu za uwekezaji, ili kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ushindani wa kiuchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uthabiti wa sera, uwazi wa mifumo ya utawala na ulinzi wa maslahi ya wawekezaji, kama msingi wa kujenga imani ya muda mrefu kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Rais Dkt. Samia pia ameeleza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya kimkakati, ikiwemo reli ya kisasa (Standard Gauge Railway), mtandao thabiti wa barabara, bandari za Bahari ya Hindi pamoja na bandari za maziwa makuu, kwa lengo la kuimarisha usafirishaji na kurahisisha biashara ya kikanda.
Amebainisha kuwa, Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kwa kuunganisha mtandao wake na nchi jirani kupitia bandari, reli na barabara, hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, madini na nishati.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ameainisha mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa, akiitaja kuwa ni moja ya sekta zinazoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni, sambamba na sekta nyingine za madini, nishati na kilimo.
Vilevile, ameeleza namna Tanzania inavyoshirikiana na taasisi za fedha za kimataifa na kikanda, ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia katika kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo.
Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi kupitia ubia wa kimkakati (PPP), ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


