CHAMA cha Wasioona Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kimelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuendelea kugusa maisha ya watu mbalimbali wenye mahitaji maalumu, ambapo awamu hii shirika hilo limewawezesha mtambo wa kisasa wa kutengeneza juisi. Pongezi hizo zimetolewa leo Januari 19,2025 na Katibu wa chama hicho, Bw.Vitalis Mdoe wakati akizungumza na maafisa wa NHC baada ya kupokea mtambo huo.
Amesema, mtambo huo unatarajiwa kunufaisha vikundi viwili ambavyo vina wanachama 10, hatua ambayo itawasaidia kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali. Msaada huo umetolewa leo na kukabidhiwa na Afisa Uhusiano Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NHC, Bw.Yahya Charahani kwa niaba ya uongozi wa shirika.

“Tunashukuru sana kwa ujio wenu,tulileta barua Shirika la Nyumba la Taifa kwa ajili ya kuomba mashine kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali ambavyo vinajihusisha zaidi na utengenezaji wa juisi, kwa hiyo tunashukuru NHC kwa kukubali na kuamua kutoa mashine hii kwa ajili ya vikundi hivi.”
Katibu huyo amefafanua kuwa,mashine hiyo itakuwa msaada mkubwa, huku akibainisha bado wanauhitaji mkubwa kutokana na vikundi mbalimbali walivyo navyo ambavyo vinajishughulisha na shughuli mbalimbali. Amesema, kati ya vikundi hivyo vipo ambavyo vinatengeneza sabuni, hivyo wakipata msaada kwa wadau wengine utaendelea kuwasaidia zaidi.
Aidha, wameliahidi Shirika la Nyumba la Taifa kuwa,mashine hiyo itafanya kazi iliyokusudiwa na wanatarajia siku nyingine kuwaita ili kuwaonesha matunda ya msaada huo.


Pia, Katibu huyo ameuomba ujumbe huo kumpelekea salamu za shukurani na pongezi Mkurugenzi Mkuu wa NHC,Bw. Hamad Abdallah kwa namna ambavyo ameendelea kuwa baraka kwa makundi mbalimbali ya watu wenye mahitaji maalum nchini.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NHC, Yahya Charahani amesema kuwa, mtambo huo uliotolewa na shirika utawasaidia wanachama wa chama hicho kuweza kupiga hatua na kujikwamua kiuchumi. Amesema, mradi huo ukisimamiwa vema utaleta matokeo makubwa si tu kujikwamua kiuchumi, bali kuwawezesha kutimiza malengo mengine kama makazi, ada za shule kwa watoto na kusaidia wanajamii.

Bw.Charahani amesema, Sera ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) miongoni mwa mambo ambayo inayatilia mkazo sana ni kuwapatia misaada wahitaji na imeweka mkazo mkubwa katika elimu, vijana na kusaidia katika majanga mbalimbali yanayotokea katika jamii.
Aidha, amesema, shirika hilo limetenga fungu maalum kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali katika jamii kulingana na vipaumbele ambavyo wamejiwekea kama shirika.