WATUMISHI WA MAGEREZA MANYARA WAPATIWA MAJIKO YA GESI

0
IMG-20250626-WA0042

Serikali imewapatia watumishi wa Jeshi la Magereza mitungi ya gesi na majiko ya gesi ya kupikia ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi na wananchi iliyolenga kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Hayo yamebaibishwa leo Juni 26, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu wakati wa uzinduzi wa kugawa majiko ya gesi kwa watumishi wa magereza iliyofanyika gereza la Babati mkoani Manyara.

Amesema kuwa, katika mkoa wa Manyara tayari Serikali imegawa mitungi ya gesi na majiko ya gesi yapatayo 330 kwa watumishi wa jeshi la magereza na katika gereza la Babati jumla ya majiko na mitungi 150 wamegawiwa watumishi hao wa magereza.

Amesema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia makubaliano na Jeshi la Magereza ya kuwawezesha magereza kuhama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo salama kwenda katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika magereza yote nchini.

“Kuanzia mwanzoni wa mwezi januari 2025 jeshi la magereza walishaingia kwenye matumizi ya nishati safi na salama na tayari wameachana na nishati isiyo salama na chafu kwa afya na mbaya kwa mazingira yetu, ” Ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amewataka watumishi wa jeshi la magereza kuibeba ajenda ya Mhe. Rais Samia ya kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia hapa nchini.

Katika hatua nyingine Mha. Saidy ameeleza kuwa, mifumo ya uzalishaji wa bayogesi ipatayo 126 tayari ipo mbioni kuanza kwa kushirikiana na jeshi la magereza ambayo itawezesha ununuzi wa mashine za kutengeneza mkaa mbadala 61, vile vile kuwajengea uwezo watumishi wa jeshi la magereza ya kuendeleza miradi hiyo ya nishati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza mkoa wa Manyara ACP Solomon Mwambingu amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia watumishi wa magereza majiko ya gesi na mitungi ya gesi na kusisitiza kuwa wataendelea kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia katika jamii yote inayowazunguka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *