NHC YATANGAZA NEEMA KWA WAPANGAJI WAKE

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, ameendelea na ziara yake ya kukagua hali ya nyumba za Shirika katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo leo ametembelea nyumba za gharama nafuu zilizopo eneo la Mrara, Wilayani Babati mkoani Manyara.
Katika ziara hiyo, Bw. Abdallah amekutana na kuzungumza na wapangaji wa nyumba hizo, na kuelekeza kufanyika kwa matengenezo ya haraka ili kuboresha mazingira ya makazi kwa wakazi hao. Ametoa wito kwa watendaji wa NHC kuhakikisha kuwa nyumba hizo zinakuwa safi, salama na zenye hadhi stahiki ya kuishi, akisisitiza kuwa Shirika limejikita katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa heshima na ustawi.
Kwa sasa, NHC iko katika utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya ukarabati wa nyumba zake nchini kote, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 7 kimetengwa hadi kufikia mwisho wa mwezi huu kwa ajili ya kazi hiyo. Kampeni hii inalenga kuimarisha makazi ya wateja na kurejesha hadhi ya miliki mbalimbali za Shirika.


Katika hatua ya kushangaza wengi, Bw. Abdallah pia ametangaza habari njema kwa wapangaji wa nyumba hizo – kuwa sasa wanaweza kuzinunua nyumba wanazoishi kupitia mpango wa Mpangaji Mnunuzi (Tenant Purchase Scheme). Kupitia mpango huu wa kipekee, kodi anayolipa mpangaji kila mwezi itahesabika kama sehemu ya malipo ya muda mrefu ya ununuzi wa nyumba hiyo.
Mpango huu ni sehemu ya dhamira ya NHC ya kuwawezesha Watanzania kumiliki makazi yao kwa njia nafuu na rahisi, hasa kwa wananchi wa kipato cha kati na cha chini. Kwa mara nyingine tena, NHC imeonesha kuwa si tu mtoaji wa makazi bora, bali pia mshirika wa kweli katika kutimiza ndoto za Watanzania kumiliki nyumba zao.