WANANCHI WAONESHA UTAYARI KWA MRADI WA MEDELI PHASE III

Wananchi wa Jiji la Dodoma na mikoa jirani wameonesha utayari mkubwa wa kuchangamkia nyumba za mradi mpya wa Medeli Awamu ya Tatu (Medeli Phase III), unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dodoma.
Katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park kuanzia Juni 16 hadi 23, 2025, maofisa masoko na biashara wa NHC walipata fursa ya kuwaeleza wananchi kuhusu faida na ubora wa mradi huo.
Kwa mujibu wa maelezo yao, mradi wa Medeli Phase III unalenga kujenga makazi ya kisasa yenye mandhari ya kuvutia, maegesho ya kutosha, usalama wa uhakika na mazingira bora kwa kuishi au kuwekeza.

Maadhimisho haya yalifunguliwa rasmi tarehe 17 Juni 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa George Simbachawene, na kufungwa leo tarehe 23 Juni 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hotuba yake ya kufunga maadhimisho hayo, Mheshimiwa Majaliwa alizindua mifumo miwili ya kidijitali:
Government Enterprise Service Bus (GovESB): Mfumo wa kielektroniki unaowezesha mifumo ya serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi.
e-Wekeza: Mfumo unaomuwezesha Mtumishi wa Umma kuwekeza moja kwa moja katika Mfuko wa Faida (Faida Fund).

Siku ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango muhimu wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.”