KINYOZI AENDA JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA MWANAFUNZI

0
1002273365

Mahakama ya Wilaya ya Kwimba imemhukumu Lindwa Clement Balthazari (30), mkazi wa kijiji cha Malya na kinyozi wa saluni ya kiume, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 14 kutoka Shule ya Msingi Mwakulilima (jina linahifadhiwa kwa sababu za kisheria).

Hukumu hiyo imesomwa , Juni 17, 2025, na Hakimu Mkazi Mfawidhi Ndeko Dastan Ndeko katika kesi ya jinai namba 31961/2024, baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 4, 2024, na kusomewa shtaka la kubaka na Wakili wa Serikali Juma Kiparo, ambapo alikana kutenda kosa hilo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Lindwa alitenda kosa hilo nyumbani kwake kwa nyakati tofauti mwezi Oktoba 2024, akitumia nafasi ya kumhudumia mtoto huyo kwenye saluni yake kabla ya kumrubuni na kumbaka, kinyume na vifungu vya sheria 130(1), 130(2)(e), na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (marejeo ya 2022).

Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi wanne, wakiwemo mhanga na daktari, kuthibitisha pasipo shaka tuhuma hizo. Mtuhumiwa alijitetea kuwa alimchukua binti huyo kwa lengo la kumsaidia baada ya kufukuzwa nyumbani, hoja ambayo ilitupiliwa mbali na Mahakama.

Jitihada zake za kuleta mashahidi watatu kwa ajili ya utetezi hazikufua dafu, na Mahakama ikamhukumu kifungo hicho ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *