WAZIRI SIMBACHAWENE AIPONGEZA WIZARA YA MADINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Simbachawene ameipongeza Wizara ya Madini kwa kazi nzuri inayofanya hususan katika kuendeleza Sekta ya Madini pamoja mikakati mizuri inayoendana mabadiliko ya sayansi na teknoloji.
Simbachawene ametoa pongezi hizo leo Juni 17, 2025 alipotembelea banda la Wizara ya Madini lililopo katika viwanja vya chinangali kwenye maonesho ya Utumishi wa Umma 2025.
Simbachawene amesema kuwa, kulingana na takwimu zilizopo zinaonesha jinsi Sekta ya Madini inavyopiga hatua kubwa hasa katika kuvutia uwekezaji ndani ya nchi.


Kuhusu uongezaji thamani madini mbalimbali, Simbachawene amekipongeza kituo cha Jiomolojia Tanzania (TGC) kwa kazi nzuri ya uongezaji thamani madini na miamba ambayo inatoa bidhaa mbalimbali zinazotumiwa na watanzania katika matumizi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.
Mapema baada ya kutembelea mabanda mbalimbali Simbachewene amefungua rasmi maonesho ya Utumishi wa Umma kwa kuwataka watumishi wa Umma kufanya kazi kwa kuzingatia matumizi ya Mifumo ya Kidigitali ili kuongeza Upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika ni siku maalum ya Watumishi wa Umma na taasisi za Umma ambayo husherehekewa kuanzia Juni 16 hadi 23 kila mwaka na nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya Bara la Afrika.

Chimbuko la Sherehe hizi ni uamuzi wa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma uliofanyika Tangiers nchini Morocco mwaka 1994.
Uamuzi huu ulizitaka nchi za Afrika kusherehekea sherehe hizo kwa kauli mbiu moja katika Bara zima la Afrika.