BUNGE LAPITISHA MUSWADA WA SHERIA YA SHIRIKA LA NYUMBA

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa mwaka 2025.
Muswada huo umesomwa leo Juni 9, 2025 bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi ambapo umelenga kurekebishwa kwa kuongeza majukumu mapya na kuboresha majukumu yaliyopo ya bodi ya Shirika ambayo imekuwa ikiyatekeleza lakini yalikuwa hayajabainishwa katika sheria.
Baadhi ya vifungu vimependekezwa kurekebishwa ikiwa ni kuweka mamlaka ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu kuwa ni Rais badala ya Waziri pamoja na kuboresha masharti ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, ambapo lengo la marekebisho hayo ni kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika usimamizi wa shirika.

Aidha, vifungu vingine vimependekezwa ikiwemo kupanua wigo wa nyaraka ambazo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo kuweza kukasimisha mamlaka ya kuzisaini kwa maafisa waandamizi wa shirika hilo ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya shirika kwa wakati.
Pia, imependekezwa kurekebishwa kwa wajibu wa mwajiri kukata kiasi cha fedha ya kodi ya nyumba pamoja na faini ya kuchelewesha kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi, ambaye ni mpangaji wa Shirika ili kulipa kodi ya pango kama ambavyo wapangaji binafsi wanalipa.