NHC YAPONGEZA MPANGO WA TET WA KUWAPATIA WANAFUNZI VITABU NA KOMPYUTA

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepongeza mpango wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wa kuwapatia wanafunzi vitabu vya kiada na kompyuta maalumu, na limeahidi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa mafanikio.
Maelezo hayo yametolewa leo katika Makao Makuu ya NHC, Kambarage House, baada ya viongozi wa taasisi hizo mbili kukutana kwa ajili ya kujadili namna ya kushirikiana katika sekta ya elimu. Mpango huo wa kitaifa, unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 27 Juni 2025, unalenga kuboresha ujifunzaji kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, shirika lake linaunga mkono kikamilifu juhudi za TET, na liko tayari kutoa mchango wa kitaalamu, kiufundi na kifedha. Alisema kuwa mpango huo unaendana na dira ya taifa ya kuinua kiwango cha elimu na maendeleo kwa ujumla.
Mpango huo utaanza kutekelezwa kwa awamu katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watapatiwa vitabu vya kiada, na wale wa kidato cha tano na sita watapatiwa kompyuta zitakazowawezesha kutumia teknolojia katika kujifunza.
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, alisema mpango huo umeandaliwa ili kukabiliana na changamoto za uhaba wa vitabu na vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi. Pia utahusisha mafunzo kwa walimu kuhusu matumizi ya teknolojia (TEHAMA) darasani.

Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 297 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, ikiwa ni pamoja na uchapishaji wa vitabu, ununuzi wa kompyuta na mafunzo ya walimu. Mpango huu ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya TET, ambapo kilele cha sherehe kinatarajiwa kufanyika tarehe 17 Juni 2025, chini ya ugeni rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Kwa pamoja, TET na NHC wamesisitiza kuwa ushirikiano huu utaleta mafanikio makubwa katika sekta ya elimu na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa ya kisasa yanayohitajika katika maisha na ajira.