ARUSHA MWENYEJI WA MKUTANO MKUBWA WA WAKUU WA MAJESHI WA SADC

Mkoa wa Arusha umechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa 33 wa mwaka wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mkutano unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 hadi 31 Mei 2025, na utawakutanisha viongozi wa kijeshi kutoka nchi zaidi ya kumi na tano za ukanda wa SADC.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 26, 2025 katika ofisi za Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Christian Makonda amesema kuwa Arusha imeendelea kuwa kinara wa mikutano ya kitaifa na kimataifa, pamoja na kuwa kitovu cha shughuli za utalii zinazochochea uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla akibainisha kuwa mkutano huo ni fursa nyingine muhimu kwa mkoa kuonyesha uwezo wake katika kutoa huduma bora kwa wageni wa kimataifa.
Mhe. Makonda ameeleza kuwa mafanikio haya yanatokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kudumisha amani na utulivu nchini, hali inayowavutia watalii na wawekezaji wengi kufika katika mkoa huo Arusha na kusisitiza kuwa mazingira ya utulivu ndiyo msingi wa maendeleo na kuvutia shughuli kubwa kama hizi za kimataifa.
Aidha, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano huo, ataongoza majadiliano yatakayolenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na usalama wa kikanda na watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika Mkoa wa Arusha
ambapo watoa huduma katika sekta zote wametakiwa kuonyesha ukarimu na utoaji wa huduma bora ili kuchochea uchumi kupitia fursa zitakazotokana na mkutano huo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda amewatoa hofu wananchi kuhusu uwepo wa magari na majeshi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, akibainisha kuwa hayo ni maandalizi ya kawaida ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa mkutano huo muhimu na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa utulivu na amani.