SERIKALI YAANZA KUSAMBAZA MITUNGI YA GESI YA KUPIKIA KWA BEI YA RUZUKU WANGING’OMBE


Serikali imeanza kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia 3,255 katika Wilaya ya Wanging’ombe Mkoa wa Njombe ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia nchini.
Wakati wa usambazaji wa mitungi hiyo, uliofanyika Mei 21, 2025 katika Kata ya Igwachanya wananchi wamefurahia kupata mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 19,500/- ambapo Serikali imelipia 50% ya gharama ya mitungi hiyo.
Wakizungumza wakati wa ugawaji wa mitungi hiyo, wananchi wa Kata ya Igwachanya wamesema kuwa nishati hiyo ya mitungi ya gesi itawasaidia kuharakisha shughuli ya kupika pamoja na kuwafanya wawe safi hata wakati wa kupika. Aidha, wamesema matumizi ya nishati ya gesi itawaondolea magonjwa ya kifua na mfumo wa kupumua.

Mkazi wa Igwachanya, Anita Kihombo, amesema ” kifua kilikuwa kinaniuma kwa ajili ya moshi, sasa hivi moshi hautanikuta tena, maisha yangu yatakua zaidi na zaidi” .
Naye Fadhili Zablon, mkazi wa Igwachanya amesema”Nashukuru sana kwa kupata gesi, nitakuwa naweka hela kidogo kidogo ili itakapoisha nikaongeze, wakati mwingine nitakuwa namsaidia mama kuchemsha chai na kazi ndogo ndogo za mapishi”.

Diwani wa Kata ya Igwachanya, Mhe. Antony Mawata ameishukuru na kuiomba Serikali iongeze mitungi hiyo kwa wananchi na kasi ya kusambaza ili kila mwananchi aweze kunufaika na nishati hiyo kwa bei ya ruzuku.
Akitoa elimu kuhusu nishati safi ya kupikia kwa wananchi hao, Mtaalam wa Jinsia na Nishati kutoka REA Dkt. Joseph Sambali, amesema mitungi hiyo itasambazwa katika maeneo walipo wananchi na ametoa wito kwa wakazi hao kutumia nishati safi ya kupikia ili watunze mazingira na afya zao.
