MWENGE WA UHURU WAIPONGEZA NHC MRADI WA MASASI COMMERCIAL COMPLEX – MTWARA

0
1000155257

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika jengo la Masasi Commercial Complex, mradi wa kituo cha biashara unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Halmashauri ya Mji wa Masasi, mkoani Mtwara.

Akiwa katika hafla hiyo iliyofanyika Mei 18,2025, Kiongozi huyo amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuendelea kujenga majengo ya biashara na nyumba za makazi kwa watumishi katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Masasi kwa kuwa utarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwemo huduma za kifedha katika eneo moja.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi huo, Godfrey Mkumbo, amesema jengo hilo la biashara linakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi 2,711,652,080.22 hadi kukamilika kwake, ambapo tayari kiasi cha Shilingi 1,450,718,159.94 kimeshatumika.

Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa NHC, Muungano Saguya, amesema lengo kuu la mradi huo ni kuboresha huduma kwa jamii na wafanyabiashara ndani na nje ya Masasi, pamoja na kutoa ajira za muda kwa wananchi wakati wa ujenzi na baada ya mradi kukamilika. Aidha, mradi huo unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi mbalimbali.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Masasi wamepongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa ujenzi wa kituo hicho kikubwa cha biashara karibu na makazi yao utaleta mwamko wa biashara na kuimarisha vipato vyao kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *