SEKTA YA MADINI YAKUSANYA ZAIDI YA BILIONI 902 KATI YA LENGO LA TRILIONI MOJA

0
IMG-20250515-WA0026

Mchango Wafikia Asilimia 10. 1 katika Pato la Taifa (GDP) kwa mmoja kabla ya lengo

📍 Dodoma

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amebainisha kuwa Sekta ya Madini nchini imeendelea kupiga hatua kubwa, ambapo maduhuli ya zaidi ya shilingi bilioni 902 sawa na asilimia 90.2 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni moja kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kufikia Mei 15, 2025, ikiwa ni kabla ya kumalizika kwa Mwaka wa Fedha, huku zikiwa zimesalia zaidi ya siku 45, jambo linalotoa matumaini makubwa kuwa lengo litafikiwa kwa asilimia 100.

Ameyasema hayo leo Mei 15, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa ulielekeza Sekta ya Madini ikichangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025. Hata hivyo, tayari mwaka 2024 sekta hiyo imefikia mchango wa asilimia 10.1, ikiwa ni mafanikio yaliyotangulia muda uliopangwa.

“Tumefanikiwa kuvuka lengo la kitaifa. Mwaka 2021 Sekta ya Madini ilichangia asilimia 7.3 kwenye pato la Taifa, mwaka 2023 ilifika asilimia 9.1, na hivi sasa tupo kwenye asilimia 10.1 kufikia mwaka 2024. Hili ni jambo la kujivunia,” amesema Mhe. Mavunde.

Makusanyo ya Serikali Yaongezeka kwa Kasi

Katika kipindi hicho, maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 20, kutoka Shilingi bilioni 623.24 mwaka 2021/2022 hadi kufikia bilioni 753.18 mwaka 2023/2024. Hadi kufikia Mei 9, 2025, Wizara ya Madini ilikuwa imekusanya Shilingi bilioni 902, sawa na asilimia 90.2 ya lengo la mwaka.

Upatikanaji wa Fedha za Kigeni na Ajira Nchini

Sekta ya Madini imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa upatikanaji wa fedha za kigeni. Mnamo mwaka 2023, mauzo ya madini nje ya nchi yalifikia Dola za Marekani bilioni 3.55, yakichangia asilimia 46.1 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi. Aidha, Kampuni za wazawa zimenufaika kwa kiasi kikubwa, ambapo bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na asilimia 92 ya thamani ya manunuzi yote migodini zilitolewa na Watanzania.

Kwa upande mwingine, Sekta ya Madini imezalisha ajira 19,356 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023, ambapo kati ya hizo ajira 18,853 sawa na asilimia 97.4 ni Watanzania.

Masoko na Minada ya Madini Yachochea Biashara

Waziri Mavunde ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuimarisha mazingira ya biashara ya madini kwa kuongeza idadi ya masoko na vituo vya ununuzi hadi kufikia 152 nchi nzima. Aidha, minada ya madini ya vito imeanzishwa upya baada ya kusimama tangu mwaka 2017. Mnada wa kwanza ulifanyika Desemba 2024 na wa pili Aprili 2025, ambapo madini yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.5 yaliuzwa na kuiwezesha Serikali kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 163 kupitia mrabaha, ada za ukaguzi, usimamizi na ushiriki wa minada hiyo.

Maono ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameeleza kuwa utekelezaji wa Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri unaendelea kwa kasi. Maono hayo yanalenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za madini, kuongeza upatikanaji wa taarifa za jiosayansi hususan za kina za jiofizikia, na kuhakikisha sekta ya madini inaunganishwa kikamilifu na sekta nyingine kama viwanda, kilimo, fedha na ujenzi kwa ajili ya uchumi shirikishi na endelevu.

Programu ya Mining for A Brighter Tomorrow – MBT

Aidha, kupitia programu ya Mining for Brighter Tomorrow, Serikali inatekeleza mpangoi mahsusi kwa ajili ya kuwainua wachimbaji wadogo, hususan wanawake na vijana, kuwa kuwapatia maeneo ya kuchimba na kuwasaidia teknolojia za kurahishisha shughuli zao.

Katika kuwajengea mazingira bora wachimbaji wadogo, Serikali imefuta leseni na maombi 2,648 ambayo hayakuendelezwa na ina mkakati wa kuzigawa upya kwa wachimbaji wadogo. Aidha, STAMICO imeendelea kuwalea wachimbaji hao kupitia vituo vya mfano na mitambo ya CIP, huku Kamati maalum ya watu 6 ikiundwa kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusu njia bora za kuwawezesha wachimbaji hao. Pia, mfumo wa dhamana (Credit Guarantee Scheme) umeandaliwa, sambamba na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata chumvi kwa ajili ya kusaidia wakulima wa chumvi nchini.

Mkakati wa Uongezaji Thamani Mdini Ndani ya Nchi

Kwa upande wa kuongeza thamani ya madini, Mhe. Mavunde amesema, Serikali inaendelea kuimarisha viwanda vya usafishaji ambapo hadi sasa kuna viwanda 9 vya kuchakata madini ya metali kama shaba na nikeli ikiwemo Kiwanda kikubwa cha kusafisha makinikia cha Kbanga Nickel kinachojengwa eneo la Buzwagi, ambapo vingine 6 kati ya hivyo vikitarajiwa kujengwa Dodoma.

Vilevile, Ujenzi wa jengo la ghorofa nane la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) unaendelea Jijini Arusha kwa ajili ya kuongezea thamani madini ya vito.

Mafanikio Mengine kwa Ufupi

Katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia, Jumla ya leseni za Uchimbaji Mkubwa, wa Kati na Mdogo 34,348 zimetolewa na Kampuni mbalimbali zimesaini mikataba kwa ajili ya kuanza uendelezaji wa migodi nchini.

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) nalo limepiga hatua kubwa, kutoka kutengeneza faida ya shilingi bilioni 1 kwa mwaka hadi kufikia bilioni 84 kwa mwaka ndani ya miaka mitatu,

Mafanikio hayo ni taswira chanya ya sekta ya madini, ikiwa ni uthibitisho usimamizi na miongozo inayohakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini, jambo linaloifanya Tanzania kusimama imara kama moja ya nchi zenye mifumo madhubuti ya usimamizi na ukuaji wa sekta ya madini barani Afrika na kuvutia matifa kadhaa kuja kujifunza hapa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *