RC KATAVI ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA UMEME TABORA – KATAVI

0
IMG-20250515-WA0005

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, unaotekelezwa na Kampuni ya ETDCO, ambao kwa sasa umefikia asilimia 96.

Akizungumza Mei 14, 2025, akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Katavi, Mhe. Mrindoko amewataka wananchi wa Mkoa wa Katavi, hususan wa Wilaya ya Mlele, kujitayarisha kupokea umeme kwa kujiimarisha katika shughuli za uzalishaji ili kujiongezea kipato.

Aidha, Mhe. Mrindoko ametoa rai kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufikiria kuwekeza katika Mkoa wa Katavi, kwani sasa utakuwa na umeme wa uhakika na wa kutosha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Alhaji Majid Mwanga, amewataka wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu ya umeme inayojengwa na serikali kwa gharama kubwa.

Nao wananchi wa Wilaya ya Mlele wameishukuru serikali kwa kuwaletea umeme wa Gridi ya Taifa, huku wakisema kuwa hatua hiyo itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.

Katika ziara hiyo Mhe. Mrindoko ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Alhaji Mwanga, ambapo amekagua ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora, pamoja na Kituo cha Kupokea, Kupozea na Kusambaza Umeme cha Inyonga, kilichopo Wilaya ya Mlele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *