BALOZI TOGOLANI AONGOZA UGENI WA KIND KUTEMBELEA NHC KWA AJILI YA FURSA ZA UWEKEZAJI

Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mheshimiwa Togolani Mavura, ameongoza ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo ya Miundombinu na Miji ya Nje ya Korea (Korea Overseas Infrastructure & Urban Development Corporation – KIND) katika ziara rasmi ya kutambua fursa za uwekezaji ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Ujumbe huo, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa KIND Kanda ya Afrika, Bi Ji-Hye Choi, umetembelea makao makuu ya NHC ambapo walipokelewa na Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara wa Shirika hilo, Bw. William Genya. Katika kikao hicho, Bw. Genya aliwasilisha taarifa kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana kupitia miradi ya kimkakati ya NHC, ikiwa ni pamoja na maeneo ya USA River mkoani Arusha, Uvumba jijini Dar es Salaam, na maeneo mengine yaliyoiva kwa uwekezaji katika sekta ya makazi na maendeleo ya miji.

Bi Ji-Hye Choi ameonesha kufurahishwa na kiwango cha maandalizi na utayari wa NHC katika kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa. Alieleza kuwa KIND inatafuta kwa dhati fursa ya kuanza mradi mkubwa barani Afrika, na Tanzania inaonekana kuwa na mazingira wezeshi na ya kuvutia kwa uwekezaji huo.
“Mmekuwa na maono makubwa, maandalizi mazuri, na miradi inayotekelezeka kwa haraka. Hii ni fursa ya kipekee kwetu kuanzisha ushirikiano wa muda mrefu na Shirika la Nyumba la Taifa,” alisema Bi Choi.

Kwa upande wake, Balozi Mavura alisisitiza dhamira ya serikali ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Korea Kusini kupitia uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuleta maendeleo ya miundombinu na kuinua sekta ya makazi nchini. Alitoa wito kwa mashirika na sekta binafsi Tanzania kuchangamkia fursa za ushirikiano wa kimataifa kama huu ili kuleta tija kwa taifa.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali ya Tanzania kupitia mabalozi wake, kuhakikisha inaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa nje, hasa katika sekta ya makazi, miji na miundombinu endelevu