WAHUKUMIWA MIAKA 20 GEREZANI KWA KUHUJUMU MRADI WA ETDCO

Mahakama ya Wilaya ya Lugoba, Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani, imewahukumu watu wawili, Mayunga Senteu na Muganyi Makulu, kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuiba na kuharibu miundombinu ya umeme.
Wawili hao walikutwa na hatia ya kuiba nyaya za umeme aina ya ACSR kutoka katika laini ya umeme ya kilovoti 33 (33KV), mali ya Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO).

Tukio hilo lilitokea mwaka 2024 katika eneo la Chamakweza, Kata ya Vigwaza, ambapo zaidi ya span 25 za nyaya ziliibwa kutoka kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme uliokuwa ukiendelea. Watuhumiwa walikamatwa wakiwa na viroba vya nyaya hizo na kufikishwa Mahakamani kwa kesi namba EC8785/2024.
Katika hukumu iliyotolewa Mei 8, 2025, Mahakama iliwatia hatiani na kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa kila mmoja, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na uharibifu wa miundombinu ya Taifa.