DKT. TULIA AKABIDHIWA RASMI TUZO YA HESHIMA YA MALKIA WA NGUVU

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amekabidhiwa rasmi Tuzo ya Heshima ya Malkia wa Nguvu iliyotolewa na Clouds Media Group, ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa kwa jamii pamoja na uongozi wake uliomfikisha kuwa Rais wa IPU.
Tuzo hiyo imekabidhiwa leo tarehe 16 Aprili, 2025 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainab Katimba Jijini Dodoma baada ya kuipokea kwa niaba yake tarehe 4 Aprili, 2025, katika kilele cha Hafla ya Tuzo za Malkia wa Nguvu iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Dkt. Tulia ametambuliwa kwa namna ya kipekee kutokana na juhudi zake za kuhamasisha wanawake na wasichana nchini kujiamini, kujituma na kupambana bila kuchoka ili kufanikisha ndoto zao.