NCC: UTATUZI MIGOGORO KWA NJIA MBADALA INAWEZEKANA

Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limesema usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, madai ya kimkataba na mingine iliyopo na inayojitokeza kwenye sekta ya Ujenzi, unawezekana bila wahusika wa migogoro hiyo kupelekana mahakamani.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya usuluhishi na utatuzi wa migogoro wanaotoa mafunzo kuhusu eneo hilo, chini ya uratibu wa NCC, ambapo inasaidia si tu kuokoa muda na kuacha wahusika wakiwa na amani, bali inapunguza mirundikano ya kesi mahakamani.


Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wakitoa mafunzo yaliyoandaliwa na NCC, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Dkt. Fauz Twaib ambaye ni miongoni mwa wafundisha njia hizo, amesema “Kinachotakiwa ni wasuluhishi kuzingatia maadili, sheria na taratibu za usuluhishi”.
Amesema kuwa njia zaidi ya nne za kusuluhisha migogoro mbali na kushitakiana mahakamani, zinafundishwa na kuwawezesha waliopata mafunzo hayo kuamua kwa weledi ipi inafaa kulingana na mazingira na hali halisi ya mgogoro husika.
Kwa mujibu wa Dkt. Twaib, kwa kutumia njia hizo mbadala, hakuna upande unaojeruhiwa kwa sababu pande zote zinahusika katika hatua zote muhimu za usuluhishi ikiwemo kuchagua nani ahusike kuwasuluhisha.


“Ikiwa hakuna mazingira yoyote ya tamaa inayoweza kusababisha upendeleo, mfano rushwa au chochote kile kitakachofanya usuluhishi uegemee upande mmoja, mlolongo wa kisuluhishi hautokei, hivyo kuokoa muda na gharama” amesema Dkt. Twaib.
Kwa upande wake, Mhandisi wa kujitegemea, Julius Mamiro anayefundisha mbinu hizo, hususan majadiliano ya kisuluhishi ya madai ya kimkataba ya ujenzi, amesema kuwa maadili mazuri yanafanikisha usuluhishi.
Amesema kuwa jambo kubwa wanalolisisitiza ni wataalamu wa masuala yote yanayoweza kuhusika kwenye migogoro, iwe ya sekta ya ujenzi au sekta yoyote, muhimu kuwa na elimu ya namna ya kutatua migogoro yao bila kupelekana mahakamani pamoja na kutekeleze mbinu walizofundishwa kwa kuzingatia maadili.
“NCC inatekeleza jukumu la kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wengi, kwa faida ya wanaoipata, wateja wao, familia zao na Taifa kwa ujumla” amesema Mhandisi Mamiro.
Amesema kuwa, kutokana na umuhimu huo, amewashauri watanzania kuchangamkia mafunzo hayo pindi wanapopata fursa wakati wote inapotangazwa.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anayehusika na sehemu ya mikataba, majadiliano na utawala, Mkadiriaji Majenzi Elias Kisamo, pamoja na kufundisha, alijibu maswali yaliyoulizwa na washiriki wa mafunzo hayo, na kuongeza uelewa wao juu ya walichojifunza.
“Ukitaka usuluhishi uende sawa, epuka njia za mkato. Hakuna shortcuts, iwe katika majadiliano au kwenye utatuzi mwingine, epuka ‘shortcuts’…”amesema Kisamo.
Katika mafunzo hayo yaliyotolewa kwa siku tatu, washiriki walifanya mazoezi ya usuluhishi kwa vitendo na kisha kutahiniwa kwa mtihani wa kuandika, lengo likiwa kupima uelewa wao kuhusu maarifa waliyapata kwenye mafunzo hayo.