MBUNGE MALEKO AGAWA INCUBATOR KWA WANAWAKE KILIMANJARO .

0

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Esther Maleko akizungumza wakati wa kukabidhi Mashine za kutotoleshea vifaranga kwa wanawake wa kata 169 za mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya ahadi yake aliyoitoa mwaka 2020 wakati akiomba ridhaa .
Baadhi ya wanawake wakimsikiliza Mbunge Esther Maleko katika Warsha iliyoenda sambamba na utoaji wa mashine za kutotoleshea vifaranga ,warsha iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM mkoa wa Kilimanjaro 
Mbunge Esther Maleko wakifurahia muziki na wanawake waliofika kwa ajili ya kupatiwa mashine maalum kwa ajili ya kutotolesha vifaranga zilizotolewa na mbunge huyo kwa wanawake wa mkoa wa Kilimanjaro .
Mbunge Esther Maleko akikabidhi mashine maalum kwa ajili ya kutotolesha vifaranga kwa viongozi wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi wilaya za Moshi vijijini na Moshi mjini na kushuhudiwa na katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Merce Mollel .

 Anaadika Dixon Hussein – Kilimanjaro 

Katika hatua ya kuimarisha maendeleo ya wanawake mkoani Kilimanjaro, Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ester Maleko, amekabidhi mashine 169 za kutotoleshea vifaranga vya kuku (incubator) kwa kila kata ya mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya kutimiza ahadi yake ya kuinua wanawake kiuchumi kupitia ufugaji wa kuku.

Akiwa kwenye mkutano wa wanawake wa CCM uliofanyika mjini Moshi, Maleko alisema kuwa wakati wa kampeni za mwaka 2020, aliahidi kushirikiana na wanawake kuleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia miradi yenye tija, na sasa anatekeleza hilo kwa vitendo.

“Siasa ni uchumi. Mwanamke akiwa na uchumi si rahisi kuyumbishwa. Niliahidi kuwa sitakuwa mbunge wa maneno, bali wa matendo. Haya ndiyo matokeo,” alisema Maleko.

Alisema mashine hizo, ambazo zina uwezo wa kutotolesha mayai 90 kwa mzunguko mmoja wa siku 21, zimegharimu zaidi ya Sh84.5 milioni hadi sasa, na zitakwenda sambamba na mafunzo kwa vikundi vya wanawake pamoja na mitaji ya mayai ya kuanzia uzalishaji.

Katibu wa CCM: Uchumi wa mwanamke ni silaha ya kisiasa

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Molell, aliwataka wanawake kuchanganya siasa na uchumi, akisema kuwa uwezo wa kifedha kwa wanawake ni silaha muhimu ya kuimarisha chama hicho kuelekea chaguzi zijazo.

“Wanawake mnapaswa kuwa na uchumi wenu. Siasa ya maneno bila uchumi ni siasa bure. Tunataka wanawake wa Kilimanjaro wawe mfano wa kuigwa kitaifa,” alisema Molell huku akiwahamasisha wanawake kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali kuanzia Mei 1 hadi 15.

Katibu huyo alimtaja Mbunge Maleko kuwa mfano wa mwanasiasa anayetekeleza siasa ya kweli, kwa kuwa amewagusa wanawake moja kwa moja kupitia mradi unaochochea lishe bora, ajira na kipato kwa familia.

“Anachofanya si kwa ajili ya uchaguzi, bali ni utekelezaji wa ahadi. Huu ndiyo uongozi tunaoutaka ndani ya CCM – unaotatua changamoto, si wa maneno,” alisema Molell.

Aliongeza kuwa miradi kama hii itasaidia kuvunja utegemezi wa mikopo isiyolipika na kuwawezesha wanawake kujitegemea, huku akisisitiza kuwa wana CCM lazima watumie fursa kama hizi kuhamasisha na kujiimarisha katika ngazi ya mashina na matawi.

Samia apigiwa saluti

Katika hotuba zao, wote wawili – Molell na Maleko – walitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo ndani ya miaka minne ya uongozi wake.

“Tokea uhuru hadi mwaka 2020, Kilimanjaro ilipokea Sh bilioni 228 za maendeleo. Lakini chini ya Rais Samia tumepokea zaidi ya Sh trilioni 1.2 ndani ya miaka minne pekee. Hili halina mfano,” alisema Molell.

Maleko naye alisisitiza kuwa wanawake wa Kilimanjaro wako tayari kumpigania Rais Samia katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuhakikisha kura za wanawake haziyumbishwi.

“Mama Samia ametekeleza, na ametekeleza kwelikweli. Tanzania inatambua, dunia inatambua, na sisi wanawake wa Kilimanjaro tunasema: tutakupigia kura kwa nguvu zetu zote!” alisema Maleko kwa msisitizo.

Kwa mujibu wa Maleko, kila kata itapatiwa pia wataalamu watakaoendesha mafunzo ya matumizi bora ya incubator pamoja na mbinu za usimamizi wa miradi ya ufugaji wa kuku.

Wanawake waliopokea vifaa hivyo walipongeza hatua hiyo na kuahidi kuzitumia kwa tija katika kuinua uchumi wa familia zao na kuimarisha chama.

“Tumeanza na incubator, lakini tunakwenda mbele zaidi. Tutafika kila tarafa na kila kijiji. Hii siyo siasa ya msimu, hii ni siasa ya maendeleo,” alihitimisha Maleko.

Mwisho .

Anaandika Dixon Busagaga .
Moshi, Kilimanjaro

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *