ARUSHA NA KOREA KUSHIRIKIANA KWENYE UTALII WA MATIBABU NA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

0

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda leo Jumatano Machi 12, 2025 Jijini Arusha, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea Mhe. Eunju Ahn, akiialika Korea kushirikiana na Serikali katika kuukuza utalii wa Matibabu na kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana Mkoani Arusha.

Mhe. Makonda amemueleza Balozi Ahn kuwa kutokana na Arusha kuwa na ugeni mbalimbali sambamba na kuwa na Makao makuu na Ofisi mbalimbali za Kimataifa, Serikali ina maono ya Kujenga Hospitali kubwa na ya kisasa, hivyo anaamini kuwa teknolojia na utaalamu wa Korea katika matibabu unaweza kuwa chachu katika kufanikisha maono hayo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Makonda pia amemuhakikishia Balozi Ahn kuwa zipo fursa mbalimbali za kiuchumi Mkoani Arusha zinazoweza kuchangamkiwa na watu wa Korea ikiwemo sekta ya usafiri na Kilimo, akitoa hakikisho la utulivu wa kisiasa, amani na ushirikiano wa dhati kutoka serikalini kwa wawekezaji na wafanyabiashara watakaowekeza mkoani Arusha.

Katika maelezo yake Balozi Ahn, amempongeza Mhe. Makonda kwa uwajibikaji mzuri kwa wananchi sambamba na kuikuza sekta ya Utalii mkoani Arusha na kuifanya Arusha kutambulika Kimataifa, akiahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya Mkoa katika kuhakikisha maono na ndoto za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinatimia hasa katika kampeni yake ya kukuza uchumi na kuhimiza matumizi ya nishati safi hasa ya kupikia kwa wanawake wa Kitanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *