TCAA YATOA MSAADA KWA WAFUNGWA, MAHABUSU KILIMANJARO

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA) imetoa misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa wafungwa na Mahabusu wa Gereza Kuu la Karanga mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Misaada iliyokabidhiwa ni pamoja na Taulo za Kike, Sabuni, Miswaki na Dawa za meno.


Akikabidhi misaada hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw. Salim Msangi ameziomba Taasisi za Serikali na Binafsi kujenga utamaduni wa kutembelea wafungwa ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Kwa kweli niseme Taasisi zote binafsi, za Serikali tuelewe tu kwamba tuna wajibu wa kuwasaidia hawa wafungwa ambao wako hapa, kuna wafungwa na mahabusu ambao wanahifadhiwa hapa ambao wana hitaji huduma muhimu na Serikali haiwezi kufanya kila kitu hilo tulielewe,” alisema Msangi.


Ameongeza kuwa, msaada japo ni kidogo ila kwa wahitaji ni jambo kubwa sana hivyo ni jukumu la taasisi kuona umuhimu wa kusaidia kundi hilo lenye uhitaji.
Akizungumza mara baada ya kupokea misaada hiyo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro (RPO), Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Leonard Burushi ameishukuru Mamlaka hiyo na kusema misaada hiyo imekuja kwa wakati muafaka.
SACP Burushi amesema katika Gereza hilo kuna baadhi ya wafungwa na mahabusu wana mahitaji makubwa ambayo Serikali haiwezi kumfikia mtu mmoja mmoja.