SAUDI ARABIA HAWAJAPEWA BANDARI YA BAGAMOYO

Serikali ya Tanzania imesema taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba kampuni moja kutoka Saudi Arabia imepata mkataba wa uwekezaji wa kujenga na kuendesha Bandari ya Bagamoyo sio za kweli ambapo imesema kutokana na umuhimu na ukubwa wa programu ya BSEZ, umma utajulishwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wake.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Kitila Alexander Mkumbo, imesema “Serikali ipo katika hatua mbalimbali za kutekeleza programu ya ujenzi wa Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone – BSEZ), ikiwa ni moja ya miradi 17 ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26”
“Pamoja na mambo mengine, programu ya ujenzi wa Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo (BSEZ) itahusisha ujenzi wa Bandari, Kongani za Viwanda, Kongani za TEHAMA, Ukanda huru wa Biashara, na Kituo cha reli, utekelezaji wa programu hii utafanywa na Sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali kupitia mpango wa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (Public-Private Partneship-PPP)”
“Wakati Wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wameonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa miradi mbalimbali iliyopo katika programu ya BSEZ, na wapo katika hatua mbalimbali za mazungumzo na Taasisi mbalimbali husika za Serikali, Serikali haijaingia makubaliano (commitment) yoyote na Mwekezaji yeyote kwa sasa”