MIGOGORO YA NDOA, MIRATHI NA UKATILI WA KIJINSIA YATAJWA KUTAWALA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA
Kampeni ya utoaji wa Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ijulikanayo kama ‘Mama Samia Legal aid Kampeni’ inaendelea na utekelezaji wake katika Mikoa sita Nchini ambapo kuanzia tarehe 24 Januari, 2025 jumla ya Mikoa 6 inatarajiwa kufikiwa na Kampeni ambayo itafanyika katika Halmashauri zote za Mikoa hiyo na kuzifikia Kata kumi kwa kila Halmashauri.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 20 Januari, Jijini Dodoma Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema mpaka sasa Kampeni hiyo imeshawafikia Watanzania Wanyonge takribani 775,119 wakiwemo Wanawake 380,375 na Wanaume 394,744. Aidha Jumla ya Migogoro 693 imetatuliwa na kuhitimishwa kati ya migogoro 3,162 iliyopokelewa katika Mikoa 11 iliyofikiwa na Kampeni.
“Kampeni ya Msaada wa Kisheria ni mkombozi mkubwa kwa Wananchi Wanyonge na wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili na mfumo mzima wa Sheria.Kupitia Kampeni hii Wanyonge wanasaidiwa kupunguza malalamiko katika sekta ya Sheria kwa kusimamia kikamilifu Sheria ya Utoaji Haki.”Alisema Waziri Dkt. Ndumbaro
Jumla ya Mikoa sita inatarajiwa kufikiwa na Kampeni hii kuanzia tarehe 24 Januari, 2024 ikiwemo Kigoma, Kilimanjaro, Geita, Katavi, Tabora na Mtwara na kuzifikia Kata kumi kwa kila Halmashauri za Mkoa tajwa.
Hata hivyo, Maeneo ya Ukatili wa Kijinsia,Migogoro ya Ndoa, Mirathi, na Ardhi yamebainika kuwa ni maeneo yenye changamoto kubwa kwa Wananchi wakati wa utekelezaji wa Kampeni hiyo.