DC NZEGA AWALIPIA GHARAMA ZA KUUNGANISHA UMEME WANANCHI
Katika kuunga mkono kampeni ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya kuhamasisha wananchi kuunganisha umeme kwenye nyumba zao, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai amewalipia gharama za kuunganisha umeme wazee na wenye ulemavu katika Kijiji cha Nzogolo Kata ya Nzega ndogo.
Mkuu huyo wa Wilaya alitoa ahadi hiyo wakati wa kampeni inayoendelea Mkoa wa Tabora inayotekelezwa na REA ya kutoa elimu kwa umma na kuhamasisha wananchi waliofikiwa na miradi ya umeme vijijini wanaunganisha nyumba zao na umeme.
“Tunampongeza na kumshkuru sana Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea umeme vijijini na sasa anapeleka kwenye vitongoji. Ni jukumu langu mimi na wewe kutumia fursa hii adhimu kuunganisha umeme. Na mimi kama mwakilishi wa Mhe. Rais nitawawekea wazee wangu wa hapa wawili, kuna mama nimetoa fedha pia awekewe umeme,” amesema Mhe. Tukai.
Mhe. Tukai pia amewahamasisha wananchi kutumia umeme huo kujiletea maendeleo kwa kufanya shughuli zitakazowaongezea kipato kupitia uwepo wa umeme huo huku akiwataka kutunza miundombinu hiyo ya umeme.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Tabora, Mha. Oscar Migani amesema Serikali kupitia REA imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 53.97 kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati vijijini katika Wilaya ya Nzega.
Katika Mkutano huo, Mbunge wa Nzega Mjini ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe aliahidi kuwalipia wananchi 10 ili waunganishiwe umeme kwa lengo la kuhamasisha shughuli za maendeleo katika Kata hiyo.