MAFUNZO UBORESHAJI WA DAFTARI MIKOA YA MTWARA, LINDI NA RUVUMA YAFUNGULIWA LEO
Mwenyekiti wa tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 17 hadi 18 Januari, 2025 Mkoani Mtwara ambapo amewataka watendaji hao kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili viweze kutumika katika maeneo mengine nchini pamoja na kuzangitia mafunzo hayo ili wakafanikishe zoezi hilo muhimu.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura mkoani humo linataraji kuanza Januari 28,2025 na kufikia tamati Februari 03,2025 huku vituo vikitaraji kufunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:jioni kwa siku zote saba.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi, Ndg. Kailima, R. K akizungumza jambo wakati wa mafunzo hayo.
Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara, Fredrick Mwanamboje akiwasilisha mada ya uraia kwa watendaji wa uboreshaji mkoa wa Mtwara wakati wa mafunzo ya siku mbili ya watendaji hao ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura mkoani huo. Watendaji hao ni pamoja na Mratibu wa Uandikishaji wa Mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa Halmashauri.
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk leo tarehe 17 Januari, 2025 amefungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ngazi ya mkoa, mkoani Lindi ambapo amewataka watendaji hao kutunza vifaa vya uboreshaji wa Daftari na kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume wakati wote wa utendaji wao.Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa huo ambao utafanyika sambamba na Mkoa wa Mtwara na mkoani Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Madaba, Namtumbo na Tunduru kuanzia tarehe 28 Januari, 2025 hadi tarehe 03 Februari, 2025 na ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Na Waandishi wetu,Mafunzo kwa Watendaji wa uchaguzi katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma katika halmashauri za wilaya ya Madaba, Namtumbo na Tunduru ikiwa ni mzunguko wa 10 wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yamefunguliwa leo mkoani Mtwara na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jacobs Mwambegele.
Mafunzo kama hayo pia yamefunguliwa katika mikoa ya Lindi na Ruvuma ambapo mkoani Lindi mafunzo hayo yamefunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk na mkoani Ruvuma, mafunzo hayo yamefunguliwa na Mjumbe wa Tume Mhe. Magdalena Rwebangira.
Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 17 hadi 18 Januari, 2025 Mkoani Mtwara Mhe. Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili viweze kutumika katika maeneo mengine nchini.
Amesema ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini.
Mkoani Lindi, Makamu Mwenyekiti wa Tume Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk amewaambia watendaji hao kuwa wakati wa uboreshaji wa Daftari katika mikoa hiyo, mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.
Amewaambia watendaji hao kuwa wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.
Hata hivyo Mhe. Jaji Mbarouk amesisitiza kuwa mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangira ambaye amefungua mafunzo hayo kwa watendaji wa uboreshaji katika mkoa wa Ruvuma ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea umahiri watendaji hao ili waweze kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watakaohusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Ameongeza kuwa Maafisa TEHAMA nao watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa muda wa siku mbili ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma katika halmashauri za wilaya ya Madaba, Namtumbo na Tunduru ambao utafanyika kuanzia tarehe 28 Januari, 2025 hadi tarehe 03 Februari, 2025.
Mratibu wa Uandikishaji wa Mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa Halmashauri wamekula kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kile cha kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoa wa Mtwara, Mhe. Lucas Jang’andu ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuanza kwa mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa uboreshaji ngazi ya mkoa katika Mkoa wa Mtwara.