MIFUMO YA ZAJI WA NAFAKA NA MAZAO MCHANGANYIKO ITAKUZA SEKTA YA KILIMO
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela amesema mifumo ya uuzaji wa mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko itaimarisha ukuaji wa sekta ya kilimo na kumlinda mkulima dhidi ya unyonyaji hususan kwenye bei na vipimo.
Mhe. Shigela ameyasema hayo mjini Geita leo tarehe 8 Januari 2025 walipokutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao mchanganyiko (COPRA) Bi. Irene Mlola.
Mheshimiwa Shigela amesema mkoa wa Geita unaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kupitia (COPRA) katika kurasimisha biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko kwa kuweka mazingira ya kuhakikisha mkulima ananufaika na kazi ya mikono yake.
Awali akizungumza na Mhe. Shigela, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Bi. Irene Mlola amesema mamlaka imeshaanza kuweka wataalamu wake watakaoshirikiana na wataalamu wengine katika mikoa ya kanda ziwa ili kuhakikisha biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko inafanyika kwa kufuata mifumo kama ilivyoelekezwa na serikali.
Aidha Mkurugenzi Mlola amesema wataalamu wa COPRA watafanya kazi ya kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanakuwa na ubora kwa mujibu wa mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Malaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao mchanganyiko (COPRA) anaendelea na ziara ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo pamoja na kazi zingine anatambulisha uwepo wa maafisa wa mamlaka kwa lengo la kuweka mazingira ya utendaji kazi wa pamoja ili kuendesha shughuli za biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko yanayolimwa katika mikoa ya kanda ya ziwa.