SIMIYU IPO TAYARI KUSHIRIKIANA NA COPRA KATIKA MATUMIZI YA MIFUMO BORA YA MASOKO YA MAZAO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi amesema yupo tayari kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko COPRA kuhakikisha mifumo ya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko inafuatwa kama ilivyoelekezwa na serikali.
Mhe. Kihongosi ameyasema hayo leo tarehe 7 Januari, 2025 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko Bi. Irene Mlola alipofika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutambulisha uwepo wa watumishi wa mamlaka hiyo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwemo mkoa wa Simiyu.
Mkurugenzi mlola amemueleza Mhe. Kihongosi kuwa COPRA itafanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wote kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji ili kuhakikisha pamoja na mambo mengine, masoko ya nafaka na mazao mchanganyiko yanafanyika kwa kufuata miongozo iliyowekwa na serikali ya matumizi ya stakabadhi za ghala na uuzaji kwa njia ya minada ya kidigitali hususani kwa Mazao ya Dengu, Choroko, Mbaazi, Karanga, Ufuta, Iliki, Karafuu, pilipili manga, Kakao, soya na mdalasini.
Mkurugenzi Mlola ameongeza kuwa serikali imeweka taratibu rasmi za biashara hizo kwa lengo la kuinua wananchi kiuchumi wakiwemo wakulima ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiuza mazao yao kwa bei ya chini ukilinganisha na gharama za uzalishaji. Pia wamekuwa wakiathiriwa na kutokutumika kwa vipimo rasmi vilivyothibitishwa na kutambulika na mamlaka za serikali.
Aidha Bi. Mlola amesema COPRA kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itahakikisha wakulima wanapatiwa maarifa ya uzalishaji wa mazao bora kwa kuzingatia mahitaji ya soko la mazao ndani na nje ya nchi.