ULEGA AMKABIDHI MKANDARASI UJENZI WA DARAJA LA TANGANYETI LILILOATHIRIWA NA EL- NINO

0

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemkabidhi Mkandarasi Jiangx Geo Engineering kazi ya ujenzi wa daraja la Tanganyeti wilayani Longido lenye urefu wa mita 40 katika barabara ya Arusha-Namanga ambapo zaidi ya shilingi bilioni 4.6 zitatumika katika ujenzi huo.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Wilayani Longido mkoani Arusha na kusisitiza ujenzi wa daraja hilo kukamilika kwa wakati ili kurahisisha mawasiliano ya Barabara ya Arusha – Namanga inayounganisha Tanzania
na Kenya.

“Barabara hii ni barabara ya utalii hivyo ujenzi wake ufanyike usiku na mchana ili ukamilike kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi”, amesema Ulega.

Aidha Waziri Ulega amezungumzia umuhimu wa taasisi zinazojenga barabara TANROADS na TARURA kushirikiana, kujenga barabara zenye viwango na kuzingatia thamani ya fedha ili kuleta tija na kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi katika miji na majiji nchini.

“Arusha ni mji wa utalii hivyo lazima uwe na barabara nzuri, salama, zenye taa, zisizo na msongamano zinazopitika wakati wote na hivyo kuchochea maendeleo”, amesema Ulega.

Waziri Ulega ameitaka TANROADS kutumia taa za umeme wa jua (solar power), ambao ni nafuu na kuuacha umeme wa Tanesco kutumika kwenye kazi nyingine za uzalishaji.

“Mhe. Rais Samia analeta fedha nyingi kwaajili ya miundombinu hivyo ushirikiano baina ya taasisi hizi utachochea kasi ya ujenzi na kukuza uchumi wa wananchi.

Amemhakikishia Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda kuwa Serikali itazijenga barabara zote unganishi na wezeshi jijini Arusha ili kupunguza msongamano wa magari na kuendana na maandalizi ya mashindano ya kombe la mataifa ya Africa AFCON 2027.

Naye mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda amesema idadi ya magari jijini Arusha imeongezeka mara kumi kutokana na ufanisi wa bandari ya Tanga hivyo upanuzi wa barabara jijini Arusha utaleta tija kwa huduma ya usafiri na uchukuzi.

Mtendaji mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amesema wamejipanga kuhakikisha miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja inayoendelea mkoani Arusha itakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.

Daraja la Tanganyeti likikamilika litakuwa na uwezo wa kupitisha uzito wa tani 80 na ujenzi wake utatumia siku 365 .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *