WAZIRI NDUMBARO ATOA MSAADA WA KISHERIA GEREZANI
Kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 14 Desemba 2024, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ametembelea Gereza la Kiberege lililopo Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro, ambapo ameongoza zoezi la utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu kupitia ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’.
Katika zoezi hilo, Waziri Ndumbaro ametoa msaada wa kisheria kwa wafungwa kumi na tano na mahabusu wawili, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wafungwa na mahabusu wote, hususan wale waliofungwa kwa makosa ya kusingiziwa.
Amewahakikishia wafungwa kwamba Serikali inaendelea kujizatiti kutoa msaada wa kisheria kwa wale wanaohitaji huku akiwasisitiza wale waliofungwa kwa makosa halali, watubu makosa yao na wakawe raia wema pindi watakapo maliza vifungo vyao.
Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), inajipanga kuanzisha kambi maalumu ya mawakili watakaotembelea magereza zote nchini kwaajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa.
Ameagiza kambi hiyo ianzie katika Gereza la Kiberege, ambapo mawakili wa TLS watajizatiti kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa wenye changamoto mbalimbali za kisheria.
Aidha, kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria Bila Malipo ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ inaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya Iringa, Mara, Songwe na Morogoro.
Jumla ya Mikoa 11 imeshafikiwa na huduma hiyo, na lengo ni kuwafikia wananchi wa Mikoa yote nchini, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.