ZAIDI YA BILIONI 3 ZIMETENGWA KURASIMISHA MAKAZI JIJINI DAR ES SALAAM
Serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 3 kurasimisha makazi ya wananchi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika kukamilisha zoezi hilo, Waziri a Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha hadi kufikia Januari 2025 alama za upimaji “Beacon’ 40,000 ziwe zimesimikwa kwenye ardhi na kuwarasimishia wananchi makazi yao ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo Desemba 13, 2024 wakati wa uzinduzi wa ukwamuaji urasimishaji makazi awamu ya pili Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo, hati 200 za viwanja zimekabidhiwa kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga na Segerea katika Mkoa wa Dar es Salaam na kusisitiza zoezi hilo kutekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza zoezi la urasimishaji wa makazi yaliyojengwa bila kupangwa ambapo hadi kufikia Novemba 2024, jumla ya mitaa 270 ya Halmashauri tano za mkoa huo zinatekeleza miradi ya urasimishaji kutokana na kuwa na tatizo kubwa la makazi yasiyopangwa.
“Ndugu zangu Wananchi wa Dar es Salaam, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa zoezi hili ametenga zaidi ya Sh Bilioni 3 kwa ajili ya mradi huu wa urasimishaji ili kuondoa tatizo hili la makazi mengi yasiyopangwa na kuongeza thamani ya ardhi yenu wananchi.
“Hivyo, naelekeze hadi kufikia Januari 2024, alama za upimaji ‘beacon’ 40,000 ziwe zimesimikwa kwenye ardhi na kuwarasimishia wananchi makazi yao. Na ifikapo Juni 2025, kila mwananchi awe amerasimishiwa eneo lake na ‘beacon’ zikiwa zimewekwa,” amesema Mhe Ndejembi.
Aidha, amewataka watendaji watakaotekeleza zoezi hilo la ukwamuaji urasimishaji kuzingatia weledi, sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu.
“Sitarajii kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ya kwamba watendaji wetu mnaenda kinyume na utaratibu kwenye zoezi hili, na mtumishi yeyote ambaye ataenda kinyume na kutotenda haki tutamchukulia hatua kali za kinidhamu,” amesema Mhe Ndejembi.