BASHUNGWA AHITIMISHA LIGI YA KASEKENYA CUP 2024 – ILEJE
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amehitimisha kwa kishindo Ligi ya mpira wa miguu Kasekenya Cup’ iliyoandaliwa na Mbunge wa Ileje, Eng. Godfrey Kasekenya ambapo timu ya Iyuli kutoka Mlal iliibuka bingwa baada ya kuifunga timu ya Jibanda kutoka Lusisi kwa penati 5 kwa 3 baada ya kutoka sare ya goli 1 kwa 1 katika dakika 90 ya mchezo.
Mashindano hayo yaliyoshirikisha jumla ya timu 84 yamehitimishwa katika Uwanja wa Mwenge uliopo Wilayani Ileje Mkoani Songwe kwa kushuhudiwa na viongozi wa Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na wananchi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo.
Awali,Finali hizo zilitanguliwa kwa kumtafuta mshindi wa tatu kwa mchezo kati ya timu ya Kimbunga FC kutoka Itale iliyoifunga timu ya Isoko kwa Penati 4 kwa 3 baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 za mchezo.
Akizungumza na wananchi wa Ileje, Bashungwa amempongeza Eng. Kasekenya kwa udhamini na kufanikisha mashindano hayo kwa wananchi wa Ileje na kusisitiza kuwa michezo ni fursa kwa vijana kuimarisha afya, umoja na kuibua vipaji ambapo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
“Nikupongeze Mheshimiwa Kasekenya kwa kuendesha hii ligi na kuifanikisha kama tulivyoshuhudia, nikuahidi tutaendelea kukuunga mkono kwa asilimia mia moja hata katika ligi nyingine ya mwakani”, amesema Bashungwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ileje, Eng. Godfrey Kasekenya, amewashukuru wananchi wa Ileje kwa ushiriki katika michuano ya ligi hiyo ambayo ilianza katika vijiji 71 na timu zote zilipata fursa ya kushiriki ligi hiyo na kwenda katika Kata 18 pamoja na Tarafa 2 ambapo katika kila mchezo kila mshindi alipata zawadi.
Mashindano ya Ligi ya Kasekenya yameshirikisha michezo mbalimbali ikiwemo Soka la wanaume na wanawake, muziki wa dansi, ngoma za asili, riadha na kukimbiza kuku ambapo washindi wametunukiwa zawadi mbalimbali ikwemo Kombe, Jezi, Medali ya Shaba, zawadi ya mipira na Fedha Taslim.