MRADI WA UMEME WA RUSUMO WAFIKIA ASILIMIA 99.9

0

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Nishati wanaosimamia Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mawaziri wa nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda wamekutana na kujadiliana kuhusu mradi huo ambao upo karibuni kuzinduliwa.

“ Mradi umefikia asilimia 99.9 na vimebaki vitu vichache ili kuukamikisha, katika kikao cha Baraza la Mawaziri kuhusu mradi tumekubaliana kuwasilisha maombi yetu kwa wakuu wa nchi ili watakapota nafasi mwakani mwezi wa pili waweze kuzindua mradi huu,” amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema kuwa kwa sasa nchini Tanzania mahitaji ya juu ya umeme ni Megawati 1,800 na kuna uwezo wa kuzalisha Megawati 3,070 hivyo kuna ziada ya umeme.

Amesisitiza “ Kuwa na vyanzo vingi ya umeme maana yake tunakuza uchumi wa nchi yetu, asilimia 52 ya umeme wote tunaozalisha unatumiwa na wananchi na asilimia 48 inatumika kwenye viwanda.”

Dkt. Biteko ametaja manufaa ya mradi huo kuwa hadi sasa umezalisha ajira kwa watu pamoja na kusaidia uwepo wa miradi mbalimbali kwa ajili ya huduma kwa jamii (CSR) hususan katika Halmashauri ya Ngara. Aidha, mradi huo umeiunganisha Tanzania na nchi za Rwanda na Burundi na pia unatoa fursa ya kuziuzia umeme nchi hizo endapo zitahitaji licha ya uwepo wa megawati 27 zinazopatikana kwa kila nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametoa wito kwa jamii kuutunza mradi huo ili uweze kuendelea kutoa umeme “ Mradi huu hauwezi kuwa wa kudumu kama hatutunzi mazingira na leo tumetoa maelekezo kwa Baraza tuanze kupanda miti katika eneo la mradi ili kuendelea kutunza mazingira na kuwa na vyanzo vya uhakika vya umeme,”

Imeelezwa kuwa, mradi wa huo wa kufua umeme unaotokana na maji wa Rusumo, umeanza kuzalisha megawati 80 ambazo zinagawanywa kwa usawa wa megawati 27 kwa nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi na hivyo kuzidi kuimarisha gridi za Taifa za umeme.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Umeme ya Rusumo (RPCL) inayomilikiwa na nchi zote tatu ni kielelezo cha azma ya Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *