NHC YAKABIDHIWA CHETI CHA SHUKRANI NA JUKWAA LA WAHARIRI

0

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepokea Cheti cha Shukrani kwa mchango wake mkubwa kama mmojawapo wa wamdhamini wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 8 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, unaofanyika jijini Dar es Salaam. Cheti hicho kimekabidhiwa kwa heshima na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicolaus Mkapa, kwa Meneja wa Habari na Uhusiano wa NHC, Bw. Muungano Kasibi Saguya.

Katika hafla hiyo ya kukabidhi cheti, Bw. Mkapa aliipongeza NHC kwa kujitolea kusaidia mikutano ya aina hii, ambayo inaleta pamoja wadau muhimu wa sekta ya habari na maendeleo nchini. Alisisitiza kuwa mchango wa NHC katika kufanikisha mkutano huo umeimarisha mshikamano kati ya sekta binafsi na ya umma, kwa lengo la kuboresha ustawi wa sekta ya habari nchini Tanzania.

Mkutano huu wa siku nne ulioanzia tarehe 6 hadi 9 Novemba, ulihudhuriwa na viongozi wa juu serikalini, wawakilishi wa mashirika ya umma na binafsi, na wadau mbalimbali wa sekta ya habari. Lengo kuu la mkutano lilikuwa kujadili na kubuni mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazokabili sekta ya habari nchini, pamoja na kuhimiza uwekezaji na ushirikiano kati ya wadau wa sekta hiyo.

Bw. Saguya, akipokea cheti kwa niaba ya NHC, alieleza kuwa shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi kama hizo ambazo zina lengo la kukuza sekta ya habari na upashanaji habari nchini. Alisisitiza kuwa NHC itakuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya sekta ya habari yanayolenga kuongeza fursa za Watanzania kupata huduma bora kwa Watanzania.

NHC imekuwa mshirika wa muda mrefu wa mikutano hii ya mwaka, ikijitahidi kuhakikisha kuwa wadau wanapata nafasi ya kujadili masuala ya msingi katika sekta ya habari. Cheti hiki cha Shukrani ni ishara ya kuthamini mchango wa shirika hilo katika kuendeleza sekta ya habari na maendeleo ya jamii kwa ujumla. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *