KIKAO KAZI CHA KIMKAKATI KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI KATIKA JIJI LA TANGA – AWESO
Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa wamefanya kikao kazi cha kimkakati na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Wabunge wa Mkoa wa Tanga wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga na mjumbe wa kamati kuu ndugu Rajab Abdurahaman ikiwa ni pamoja na wenyeviti wa CCM wa wilaya zote za Mkoa wa Tanga huku lengo na madhumuni ya kikao hicho ikiwa kujadili hali ya sekta ya maji na ujenzi kwa mkoa wa Tanga.
Akizungumza katika kikao hiko jijini Dodoma waziri wa maji Mhe. Jumaa Aweso amewashukuru wabunge wa mkoa wa Tanga kwa upambanaji kwani wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri wa miradi ya kimkakati ndani ya mkoa huo.
Amesema jiji la Tanga linategemea mto Sigi na kutokana na mabadiliko ya tabianchi kina cha mto huo kinazidi kupungua hivyo ni vyema wakaanza kutafakari sasa kwa maji yatakayofika Muwenza au Pangani yaweze kuelekezewa katika jiji la Tanga kwa kuwa jiji hilo ni la viwanda na matumizi ya maji ninmengi.
“Hakuna asiyefahamu eneo la Mkata, zamani ukipita taswira ya Mkata pale yalikuwa ni madimbwi ya maji, tunatambua kabisa tulikuwa na mabwawa ya Manga yaliwekewa fedha zililiwa lakini matokeo hakuna, tulifanya kazi kubwa na nzuri hadi maji yamepatikana ambayo yanaweza kuhudumia wanamkata,
“Namshukuru Mhe. Rais kwa suala la Handeni, tumeongeza fedha kwamba tumetoka Handeni tunakwenda katika wilaya 4 na mradi zaidi wa bilioni 170 siyo jambo jepesi na miji inaenda kunufaika kwani fedha zake zipo na teki kubwa pale Handeni limekamilika.” amesema Awesoo
Aidha Aweso amesema wamefanya kikao cha viongozi wote wa chama na kuwapa mrejesho wa kazi ambayo inafanyika pamoja na kutuma timu ya wizara iliyopita kukagua miradi inayotekelezwa katika majimbo yote.
Sambamba na hayo amesema kuwa kazi ya mradi wa Handeni utatekelezwa usiku na mchana ili iweze kukamilika kwa wakati kwani fedha zimeshatengwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu Rajab Abdurahaman amesema mkoa wa Tanga umenufaika na maendeleo yatokanayo na kiwango kikubwa cha rami.
“Changamoto kwenye miradi ta barabara ni jambo ambalo lipo maeneo yote katika nchi yetu ni jambo ambalo halitamalizika kwa muda mfupi tu lakini kiukweli kwa mikakati ambayo wenzetu wa serikalini wanayo na sisi tunaridhika nayo tunaona kabisa tunakwenda kuufungua mkoa wetu wa Tanga irudi ile Tanga ambayo tunaijua sisi ikiongoza kiuchumi,” amesema Abdurahaman.