WALENGWA WA SASA KUWENI TAYARI KUHITIMU NA MUWAACHIE NA WENGINE WANUFAIKE PIA – RC MACHA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewaasa walengwa wanaonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Mkoa wa Shinyanga ambao wamefikia hatua ya kuhitimu na mpango huu kuwa tayari kuwaachia wanufaika wengine ili na wao pia wanufaike kama ambavyo wao wamenufaika.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 7 Novemba, 2024 wakati akifungua Kikao Kkazi cha kujenga uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini kwa viongozi na waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga, Simiyu, Mwanza na Kagera kikao ambacho kimefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
“Ndugu zangu wanahabari, malengo makubwa ya TASAF ni kuhakikisha wanawasaidia walengwa ambao watajinusuru na umaskini na msingi huu sasa, walengwa wote ambao kwa sasa wananufaika na tayari wamehitimu tayari wawe tayari kuwaachia na wengine ili nao wanufaike na mpango huu na hatimae waweze kuondokana na umaskini na mwisho wajikwamue kiuchumi wao na familia zao na ndiyo lengo hasa la Serikali,” amesema RC Macha.
Aidha RC Macha ameongeza kuwa lengo na hamu kubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na uongozi wake ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanaishi katika hali nzuri ya kiuchumi na kwa ustawi sawa na hatimaye kuondokana na umaskini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfumo wa Mawasiliano TASAF Makao Makuu Ndg. Japhet Boaz amesema kuwa kufikia Juni 2024 jumla ya vikundi 60,342 Tanzania nzima vyenye wananchama 838,241 vimefanikiwa kukusanya akiba ya shilingi Bilioni 7.9 na kukopeshana shilingi Bilioni 3.2 kwa ajiri ya kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali inayowaongezea kipato ili kukuza uchumi wa kaya zao.
Aidha ameongeza kuwa kaya za walengwa 84,674 zimepewa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara na kupatiwa ruzuku ya uzalishaji ambapo mpaka sasa wameanzisha shughuli za kiuchumi zenye thamani ya shilingi Bilioni 31.3 na hivyo kufanikiwa kuhitimu kwenye mpango wa kaya maskini ili kuwapisha wengine wanufaike na mpango huu.
Ikumbukwe kuwa TASAF imekuwa ikitekeleza mpango wa kunusuru kaya maskini kwa vipindi viwili (2) ambapo kipindi cha kwanza kilianza mwaka 2013 kikilenga kuhudumia kaya Milioni 1.2 na kipindi cha pili 2kilianza mwaka 2020 ambacho kimeendelea kuhudumia zaidi ya kaya Milioni 1.3 na utekelezaji wake unafanyika kwenye Halmashauri 184 za Tanzania bara na Zanzibar huku lengo kubwa ni kuwezesha kaya za walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato, huduma za jamii na kuwekeza katika kuendeleza rasilimali watu.