TAKUKURU TEMEKE WAFATILIA MIRADI YENYE THAMANI ZAIDI YA BILIONI 11.7

0

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kufatilia miradi mine yenye thamani ya shilingi 11,782,830,909 ikiwemo mradi wa ujenzi wa mtandao wa maji ambao una thamani ya shilingi 10,798,830,909 unaotekelezwa na Manispaa ya Temeke na Kigamboni.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Novemba 1, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha miezi mitatu, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke Bw. Ismail Bukuku, amesema kuwa baadhi ya miradi hiyo ilibainika na kasoro pamoja na kutolewa ushauri ili kufikia malengo.

Bw. Bukuku amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Sepemba 2024 jumla ya chambuzi za mifumo miwili zilifanyika na kubaini mianya ya rushwa ambayo ilitolewa ushauri wa namna bora ya kuziba.

Amesema kuwa katika kipindi husika wamepokea malalamiko 55, huku 50 yalihusu rushwa na matano hayakuhusu rushwa.

Bw. Bukuku amefafanua kuwa malalamiko yaliyohusu rushwa yanafanyiwa uchunguzi ili kuthibitisha tuhuma hizo, huku akieleza kuwa kuna kesi 14 zinaendelea Mahakamani.

Katika kipindi hicho TAKUKURU Mkoa wa Temeke ilishiriki katika maonesho 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa pamoja na kufanikiwa kumsaidia Bw. Mathias Paul Mazengo kupata hati ya kiwanja, kwani awali alifatilia kwa muda wa miaka tisa bila mafanikio.

‘Natoa rai kwa watumishi wa ardhi kuachana na urasimu na kuhakikisha inawahudumia wananchi wote hususan katika utoaji wa hati miliki za ardhi, TAKUKURU Temeke imefanya kazi za kuimarisha klabu za wapinga rushwa kwenye vituo vikuu na kati, shule za sekondari na msingi, imefanya mikutano ya hadhara, semina kwenye idara mbalimbali pamoja na kushiriki maonesho kwa lengo la kutoa elimu” amesema Bw. Bukuku.

Amesema kuwa lengo ni kuzidi kuelimisha jamii kuhusu rushwa ili iweze kujua wajibu wake na namna inavyoweza kushirikiana na serikali katika kuzuia vitendo vya rushwa hasa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mikakati ya TAKUKURU Mkoa wa Temeke katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu kuendelea kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi katika kukabiliana na rushwa hasa kipindi cha uchaguzi wa viongozi wa serikali za mtaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *