RAPA YOUNG THUNG AMEACHIWA HURU KWA MASHARTI
Rapa maarufu nchini Marekani kutokea jimbo la Georgia, Atalanta Jeffery Williams ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Lebo ya Muziki ya YSL ameruhusiwa kurudi nyumbani kwa masharti maalumu akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka 40.
Hukumu hiyo imekuja baada ya Thug kukaa rumande kwa takribani miaka miwili bila dhamana tangu alipokamatwa Mei, 2022 akikabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, ulanguzi wa dawa za kulevya na uendeshaji wa genge la wahuni.
Mchanganuo wa hukumu hiyo ya miaka 40 ni kama ifutavyo, kutumikia kifungo cha miaka mitano jela ikiwa ni mjumuisho wa miwili ambayo ametumikia tayari wakati wa uendeshwaji wa kesi hiyo tangu Mei 2022 ambapo miaka mitatu iliyobaki atatumikia kifungo cha ndani ya nyumba yake huku akiwa na kifaa maalumu mguuni (ankle monitor) kwa ajili ya kufuatilia nyendo zake.
Baada ya hiyo kumalizika atatumikia miaka 15 chini ya uangalizi maalumu pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii huku akipewa angalizo la kutumikia miaka 20 iliyobaki jela endapo atakiuka sharti lolote alilopewa kwenye kipindi hicho cha miaka 15.