UTORO WA MAWAZIRI SPIKA DKT. TULIA AKASIRISHWA
Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameelezea kusikitishwa kwake na kitendo cha baadhi ya Mawaziri kuendelea na tabia ya utoro na kutohudhuria vikao vya Bunge ili kujibu hoja za Serikali licha ya Rais Samia kuagiza wawepo ambapo amesema isifike mahali Bunge likawa linaahirishwa ili kusubiri Mawaziri wawepo.
Akiongea Bungeni Jijini Dodoma, Dkt. Tulia amesema “Ilikuwepo hoja kuhusu mahudhurio ya Mawaziri, ni jambo ambalo nadhani limezungumzwa mara kadhaa hapa Bungeni lakini naona sasa kuna changamoto maana wakati mwingine vikao vinaitishwa na Serikali muda wa Bunge, mwingine anaweza kuwa anafanya kikao kwa mtandao akiwa hapa Dodoma”
“Mh. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu jambo hili tumeshalizungumza mara nyingi, hata ambaye hayupo kwenye kikao anatumia hii kwamba aliitwa kwenye simu, aah Watu lazima walipe kipaumbele Bunge”
“Mh.Rais alishaagiza kipindi cha Bunge Mawaziri na Manaibu wao wawe Bungeni, ambavyo wanakuwa hawapo sote tunajua ukisema jambo moja mara nyingi na hakuna mabadiliko maana yake ni aidha unavyolisema au ni vile Mtu ameona hakuna kitu unaweza kufanya hata asipofanya”
“Bunge tunataka Serikali iwepo itusikilize tunavyotoa ushauri, kwahiyo tusifike mahali ambapo Waziri atakuwa hayupo halafu tukaahirisha Bunge ili tumsubiri yeye aje”