MIRADI CHUO CHA MICHEZO MALYA YAZIDI KUPAMBA MOTO

0

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeendelea kuweka nguvu katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya kwa kuboresha miundombinu ya Chuo hicho, pamoja na ujenzi wa Miradi ya kimkakati ili kuvutia wananchi wengi kujifunza Elimu ya michezo.

Akizungumza katika ziara ya kukagua Miradi ya Chuo hicho ambayo ni Ujenzi wa Akademia ya Taifa ya Michezo pamoja na Mabweni ya Wanachuo, Oktoba 28, 2024 , Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Methusela Ntonda amesema kuwa, Serikali imeamua kutekeleza miradi hiyo, ili Watanzania wasome na wapate utaalamu katika michezo kwa ajili ya nchi na kupata fursa za michezo ulimwenguni.

“Kwa sasa chuo hiki kimepokea fedha za miradi ya maendeleo karibu Shilingi bilioni 40 na miradi yote ipo chini ya udhamini wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kukamilika kwa miradi hii kutaongeza idadi ya Wanachuo na hivyo kupata wataalamu wengi katika sekta ya michezo” amesema Bw. Ntonda.

Amesema Wizara inatarajia kukabidhi Chuo hicho viti 600 kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa wanafunzi waliopo chuoni hapo ambao wanasoma elimu ya michezo kwa ngazi za Astashahada na Stashahada.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wanachuo na Watumishi wa Chuo hicho, wameishukuri Serikali kupitia wizara hiyo, kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo hicho na kuomba changamoto zilizopo katika Chuo hicho ziendelee kitatuliwa ili Chuo kiendane na hadhi ya kuwa Chuo pekee Cha Michezo Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *