SASA VIJIJI VYOTE MTWARA VINA UMEME
Ni furaha na nderemo kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara mara baada ya Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufanikiwa kufika umeme katika Vijiji vyote 785 katika Mkoa huo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Makome A ambacho ndio kijiji cha mwisho kuunganishwa na nishati ya umeme katika Mkoa huo leo Oktoba 28, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala ameipongeza REA kwa kufanikisha ndoto hiyo kutimia.
“Tunapenda kumpongeza sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa fedha kwa vipindi tofauti kuhakikisha historia hii inaandikwa. Sasa tuna deni kubwa kama wananchi wa Mtwara kuhakikisha tunatumia umeme huu kujiletea maendeleo yalikusudiwa,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Kanali Sawala pia amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya umeme kwa kuwa serikali imetumia gharama kubwa sana kufanikisha miundombinu hiyo kufika katika makazi yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu ametoa wito kwa wananchi wa vijiji vya mtwara kutumia kipindi hiki cha mauzo ya korosho kuhakikisha nyumba zao zinafanyiwa maandalizi ya kuingiza umeme (wiring) na kuunganisha na umeme huo wa REA ili malengo ya serikali yafikiwe.
“Gharama ya kuunganisha ni nafuu kabisa. Ni 27,000 tuu ambayo ni kodi wakati gharama zingine zote serikali imezibeba ili kuwaletea maendeleo wananchi wake. Tutumie uwepo wa umeme huu kujieletea maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza Balozi Kingu.
Awali akitoa taarifa kuhusu miradi ya REA katika mkoa huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa Wakala kupitia miradi mbalimbali iliyogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 187 imewezesha vijiji vyote 785 kupata umeme.
Mhandisi Olotu ameongeza pia baada ya kukamilika kupeleka umeme katika vijiji sasa wakala umeanza safari ya kupeleka umeme katika Vitongoji na kuwahamasisha wananchi kuendelea kutumia umeme huo kujiletea maendeleo yaliyokusudiwa.
“Mwaka 2021 vijiji 384 tuu ndio vilikuwa na umeme. Ndani ya miaka mitatu tumefanikiwa kupeleka umeme katika vijiji 401 na hivi sasa vijiji vyote 785 vina umeme. Kwenye upande wa vijiji hatuna deni. Lakini sisi kama REA hatujaishia hapo na sasa safari ya kupeleka umeme katika vityongoji imeanza.
Mkoa wa Mtwara una vitongoji 3,427 na mpaka sasa vitongoji 2,200 ndio vina umeme. Tayari tunawakandarasi wanaendelea kupeleka umeme katika vitongoji. tuwaombe wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao na Wakala kwa ujumla,” amesisitiza Mhandisi Olotu.