SERIKALI KUUNDA TIMU MAALUM KUSIMAMIA UREJESHAJI HUDUMA ZA USAFIRI WA VIVUKO MAFIA – PWANI

0

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaunda Timu Maalum itakayoshughulikia na kusimamia urejeshaji wa huduma ya usafiri wa Vivuko vya MV Kilindoni na Meli ya TNS Songosongo vinavyofanya safari kati ya kituo cha Mafia – Nyamisati (Kibiti) vilivyosimamisha huduma ya usafiri tangu tarehe 10 Oktoba, 2024.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Wilayani Mafia Mkoani Pwani wakati akikagua matengenezo ya Kivuko cha Meli ya TNS Songosongo kinachosimamiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa leo Oktoba 26, 2024

Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa huduma ya usafiri wa vivuko katika Wilaya ya Mafia ambayo imesimama kutokana na vivuko vya MV Kilindoni na Meli ya TNS Songosongo kupata hitilafu ambapo sasa kazi ya matengenezo inaendelea kwa vivuko vyote wiwili.

“Serikali ipo kazini, na kupitia timu hii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani itafanya jitihada za haraka za kurudisha huduma za vivuko viwili vya MV Kilidoni na Meli ya TNS Songosongo ili kuwaondolea adha wana Mafia ya kukosa usafiri wa Vivuko”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa Mkakati wa Serikali ni kuongeza kivuko kingine ili kusaidia wakati wa dharura kwa kutoa huduma kwa wananchi pindi kivuko kingine kinapopata hitilafu.

Aidha, Bashungwa amewahakikishia Wananchi wa mafia kuwa Timu hiyo ya Wataalam itafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanarejesha huduma za vivuko haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Ofisi yake inaendelea kuongea na Wawekezaji wa Sekta binafsi watakaoweza kufanya uwekezaji wa huduma ya Usafiri na Hoteli ili kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma hizo ambazo zitaendelea kufungua uchumi wa Wilaya ya Mafia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *