KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA JENGO LA KITUO CHA ZIMAMOTO CHA BILIONI 1.9 MTUMBA, DODOMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imetembelea na kukagua ujenzi wa jengo la kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lenye thamani ya Tsh. bilioni 1.9 katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Mhe.Vita Kawawa (Mb) pamoja na ujumbe wake amesema wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambapo amepongeza mradi huo kwa kuzingatia mambo ya muhimu kwa mahitaji ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kisima cha maji kikubwa na uwepo la tenki la akiba la kuhifadhi maji la lita laki moja na nusu.
Awali akitoa tarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) John Masunga amesema ujenzi huo ulianza Aprili 2024 ambao unagharamiwa na fedha za Serikali umefikia asilimia 50.53, huku ukitumia asilimia 34.24 ya fedha zilizotolewa.