MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI WA BILIONI 143 TABORA

0

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua wenye thamani ya shilingi Bilioni 143.26

Hafla ya uwekaji jiwe la msingi imefanyika katika mji wa Sikonge mkoani Tabora ambapo Mhe.Dkt. Mpango amesisitiza utunzaji wa miundombinu ya maji.

Amesema serikali imefanya mambo mengi makubwa kwa hiyo wananchi wanapaswa kuhakikisha miundombinu inatunzwa ili idumu kwa muda mrefu.

Mhe.Mpango ameishukuru serikali ya India kwa ushirikiano mzuri ambao umewezesha kufanikisha maendeleo kwa serikali za Tanzania na India.

Awali akizungumzia mradi huo Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amesema mradi huo ni sehemu ya mradi wa maji wa miji 28 ambao unatekelezwa kupitia mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya India. Ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandishi Mwajuma Waziri amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili 2023 na utakamilika Oktoba 2025. Amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara itaendelea kusimamia kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Amesema mradi huo utazalisha lita miliomi 24.76 kwa siku na kuhudumia zaidi ya wakazi 490,926 waliopo katika miji ya Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui pamoja na vijiji 63. Utekelezaji wa mradi huo umefika asilimia 48.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *