TUSIPOJIANDIKISHA WATACHAGULIWA VIONGOZI WASIOFAA
Ikiwa zoezi la kujiandikisha katika daftari la Makaazi limeanza leo nchini Tanzania Wananchi katika maeneo mbalimbali wamejitokeza katika zoezi hilo.
Leo Oktoba 11, 2024 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Bi. Anastazia Tutuba amewaongoza wananchi Wilayani humo kwaajili ya kujiandikisha.
Akizungumza na Wananchi hao wakati wa kujiandikisha Mkurugenzi huyo amewasisitiza wananchi kuwahamasisha wenzao ili kila mmoja ahakikishe amejiandikisha kwaajili ya kupata haki yao ya msingi kuweza kuwachagua Viongozi watakaowafaa.
“Serikali ya Mtaa ndiyo msingi wa maendeleo ya Nchi, inayosimamia maadili ya jamii, na ndiyo inayotusemea wananchi na ndiyo inayojua dhiki na changamoto za wananchi katika maeneo husika.tuhakikishe kwamba sote Kwa pamoja tunajiandikisha”
Amewataka pia baada ya zoezi la kujiandikisha wahakikishe wanajitokeza Kupiga kura na kuwahimiza wachukue nafasi za kugombea kwani wasipofanya hivyo watajitokeza wengine ambao hata sio wanaofaa kuwa Viongozi.
“Watajitokeza watagombea na mwisho watachaguana wao kwa wao na ndo watakuwa Viongozi, mwisho wa siku tutabaki tunalaumiana” amesisitiza Bi. Tutuba
Kwa Upande wao wananchi waliojitokeza kujiandikisha wameeleza kuwa zoezi hilo limekuwa zuri na hivyo wamewaomba wengine kutokupata mashaka na kwenda kujiandikisha kwani zoezi hilo halitumii muda mrefu.
Ikumbukwe kuwa zoezi hili limeanza leo 11 Oktoba, 2024 na kutamatika 20 Oktoba, 2024.